WAKURUGENZI WA KAMPUNI ZA MIPANGOMIJI WATAKIWA KUONGOZA MAGEUZI YA SEKTA

News Image Apr, 21 2026

Wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji zilizosajiliwa Tanzania Bara wametakiwa kuongoza mageuzi yatakayochochea ukuaji wa sekta ya mipangomiji na kuhakikisha miji inapangwa kwa kuzingatia viwango vinavyokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Miji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TP. Deogratius Kalimenze, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji yaliyoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji (TPRB).

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, TP. Kalimenze amesisitiza umuhimu wa kampuni za mipangomiji kuzingatia maadili ya taaluma, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Amesema kuwa uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria zinazosimamia taaluma ya mipangomiji ni msingi muhimu katika kuhakikisha miji inakua kwa mpangilio bora na endelevu.

Aidha, amewataka wakurugenzi hao kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kubaini na kudhibiti vitendo vya watu wanaojihusisha na shughuli za mipangomiji bila kufuata taratibu, ikiwemo wale ambao hawajasajiliwa na TPRB.