​WAKURUGENZI WA KAMPUNI ZA MIPANGOMIJI WAISHUKURU TPRB KWA KUWAJENGEA UWEZO
Apr, 21 2026
Wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji zilizosajiliwa Tanzania Bara wameishukuru Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) kwa kuwapa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo katika kuboresha utendaji wao wa kazi na kuongeza ufanisi katika sekta ya mipangomiji nchini.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Aprili 14, 2026 jijini Dar es Salaam, yalilenga kuwajengea uelewa wa kina viongozi hao katika masuala ya kitaaluma na kiutendaji ili kuboresha utoaji wa huduma katika kampuni zao.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, baadhi ya wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji wamesema mafunzo hayo yamekuwa chachu ya mabadiliko chanya katika uendeshaji wa kampuni pamoja na kuongeza ubora wa huduma wanazotoa kwa jamii.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Land General Planning Co. LTD, Ditrick Mbilinyi, amesema TPRB imefanya jukumu muhimu la kuziunganisha kampuni hizo kupitia mafunzo hayo, jambo lililosaidia kujenga mshikamano na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ardhicare LTD, Alloyce Nyaisa, amesema mafunzo hayo yatachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji wa kampuni, huku Modesta Kawana kutoka Ardhi Star Ltd akibainisha kuwa mada zilizowasilishwa zimewajenga kitaaluma na kuongeza uelewa wao katika sekta hiyo.
Aidha, Najum Mchunda kutoka Ardhi Institute Morogoro ameishukuru TPRB na kutoa wito wa kuendelea na mafunzo hayo hadi kwenye taasisi za elimu ya mipangomiji, wakati Gloria Kilendi wa Tupange Makazi Ltd akieleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kuendesha kampuni kwa weledi zaidi.
Naye Clemence Melo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Independent Planner Ltd, amesema mafunzo hayo yatawasaidia kutekeleza kazi za mipangomiji kwa kuzingatia viwango bora vya kitaifa na kimataifa, huku washiriki kwa ujumla wakisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa mafunzo hayo ili kuimarisha sekta ya mipangomiji nchini.


