RAIS WA TITP AIPONGEZA TPRB KWA KUWAJENGEA UWEZO WAKURUGENZI WA KAMPUNI ZA MIPANGOMIJI
Apr, 21 2026
Rais wa Chama cha Wataalam wa Mipangomiji Tanzania (TITP), Dkt. Juma Matindana, ameipongeza Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) kwa kuandaa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji zilizosajiliwa Tanzania Bara.
Dkt. Matindana ametoa pongezi hizo wakati akitoa salamu za chama hicho katika mafunzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha utendaji wa sekta ya mipangomiji nchini.
Amesema kuwa mafunzo ya mara kwa mara kwa wakurugenzi na watendaji wa kampuni ni nyenzo muhimu ya kuwajengea uelewa wa kina kuhusu taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia taaluma ya mipangomiji, hivyo kusaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha, amesisitiza kuwa uwepo wa mafunzo hayo unasaidia pia kuhakikisha kuwa kampuni zinaendeshwa kwa kuzingatia weledi, uwajibikaji na maadili ya taaluma, hali inayochangia maendeleo endelevu ya miji na makazi.
Ametoa wito kwa wadau wa sekta ya mipangomiji kuendelea kushirikiana na TPRB katika kuendeleza taaluma hiyo, ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika mafunzo na programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha sekta hiyo nchini.


