WATAALAMU MIPANGOMIJI WATAKIWA KUTOA MAPENDEKEZO MAREJEO SERA YA MAENDELEO YA MAKAZI
Jun, 17 2026
Wataalamu wa mipangomiji nchini wametakiwa kushiriki katika mchakato wa marejeo ya Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000 ili kuhakikisha sera mpya inakidhi mahitaji ya sasa na kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya makazi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TP. Deogratius Kalimenze wakati wa mafunzo endelevu (CPD) 2026 kwa maafisa mipangomiji yaliyofanyika mjini Morogoro.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB), TP. Martha Mkupasi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wataalamu wa sekta ya umma na binafsi ili kuleta maboresho endelevu katika sekta ya mipangomiji nchini.
Akifungua mafunzo hayo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro, Idrisa Juma Kayera, alieleza kuwa Serikali inaendelea kuthamini mchango wa wataalamu wa mipangomiji katika kuhakikisha miji inapangwa kwa kuzingatia usalama, ujumuishi na uendelevu ili miji iweze kupendeza.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru TPRB kwa kuandaa programu hiyo, wakisema imewapa maarifa mapya na mbinu za kisasa zitakazosaidia kuboresha utendaji wao wa kazi.


