TPRB YATOA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO WAKURUGENZI WA KAMPUNI ZA MIPANGOMIJI TANZANIA BARA

News Image Apr, 21 2026

Wakurugenzi wa kampuni za mipangomiji zilizosajiliwa Tanzania Bara wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo katika kuboresha utendaji wao wa kazi na kuongeza ufanisi katika sekta ya mipangomiji nchini.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) yamefanyika Aprili 14, 2026 jijini Dar es Salaam, yakilenga kuwajengea uelewa wa kina viongozi hao katika masuala ya kitaaluma na kiutendaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Msajili wa TPRB, TP. Martha Mkupasi, alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kutoa jukwaa kwa wakurugenzi kujadili changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameeleza kuwa kupitia jukwaa hilo, washiriki wamepata fursa ya kubaini mbinu sahihi za kukabiliana na changamoto hizo pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, jambo litakalosaidia kuimarisha utendaji na ushindani wa kampuni zao.

Aidha, Mkupasi alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha taaluma ya mipangomiji nchini, kwa kuhakikisha wataalam wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, ili kufanikisha ujenzi wa miji endelevu, jumuishi na inayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

TP. Mkupasi ametoa wito kwa wakurugenzi na watendaji wa kampuni hizo kuzingatia maadili ya taaluma pamoja na kufuata kikamilifu taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia sekta hiyo.