WATUMISHI WA TPRB WAJENGEWA UWEZO KUHUSU UANDAAJI WA VIHATARISHI NA MFUMO WA GERMIS
Aug, 14 2026
Watumishi wa Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) wamepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu uandaaji wa vihatarishi pamoja na mfumo wa kusajili vihatarishi (GERMIS), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ufanisi na uwezo wa watumishi katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mifumo ya kisasa.
Mafunzo hayo yamefanyika Jumatano Agosti 12, 2026, katika Ukumbi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mtumba jijini Dodoma, yakilenga kuwaongezea watumishi uelewa na ujuzi unaohitajika katika kutambua, kuandaa na kusimamia vihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu na shughuli za Bodi.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Msajili wa TPRB, TP. Martha Mkupasi amewataka watumishi kushiriki kikamilifu na kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kupata uelewa na ujuzi utakaowasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
TP. Mkupasi amesisitiza umuhimu wa watumishi kutumia fursa hiyo kuongeza uwezo wao na kuhakikisha maarifa wanayoyapata yanatumika katika kuboresha utendaji wa Bodi.
Akitoa mafunzo hayo, Mwezeshaji kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Onesmo Mbekenga amewapatia watumishi uelewa kuhusu namna bora ya kuandaa vihatarishi, kutathmini uwezekano wa kutokea kwa vihatarishi pamoja na athari zake, na kuweka hatua stahiki za kukabiliana navyo.


