KAMATI YA ELIMU, MAFUNZO NA WELEDI YA TPRB YAFANYA KIKAO CHA USAJILI WA WATAALAMU WAPYA WA MIPANGOMIJI

News Image Oct, 20 2025

Kamati ya Elimu, Mafunzo na Weledi ya Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) imefanya kikao chake cha 37 kujadili maombi ya usajili wa wataalamu wapya wa mipangomiji kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Kikao hicho cha siku mbili kilianza Jumatatu Oktoba 13, 2025 katika Ofisi za Bodi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, TP. Dkt. Regina John na Katibu ambaye ni Kaimu Msajili wa TPRB, TP. Martha Mkupasi, ambapo wajumbe walipokea na kujadili maombi 21 ya usajili wa wataamu wapya wa mipangomiji.

Pia, kikao hicho kilipokea na kilijadili mwenendo wa utekelezaji wa majukumu ya kusimamia taaluma na maendeleo ya taaluma, changamoto zilizojitokeza pamoja na mikakati ya kuboresha weledi na ufanisi katika taaluma ya mipangomiji.

Miongoni mwa taarifa zilizowasilishwa ni mapendekezo ya utatuzi wa changamoto za uendelezaji wa viwanda katika Mkoa wa Pwani.

Aidha, kikao hicho kilipokea taarifa ya uchambuzi wa kina wa namna ya kuwapatia mafunzo wataalamu wa mipangomiji ambao hawakupata fursa ya kupitia module za mafunzo kwa vitendo ili kuinua uwezo wao katika kutekeleza majukumu ya mipangomiji na kuwapatia sifa za kuweza kusajiliwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira.

Mwenyekiti wa Kamati, TP. Dkt. Regina John, aliwapongeza wajumbe kwa uchambuzi makini wa hoja mbalimbali na kuhimiza kuendelea kuweka mkazo katika kuinua ubora wa elimu, mafunzo na weledi katika fani ya mipangomiji, akisisitiza kuwa taaluma hiyo ni nguzo muhimu katika maendeleo endelevu ya miji na vijiji nchini.